Ads 468x60px

Jumatatu, 12 Desemba 2016

MKUU WA MKOA WA IRINGA AMINA MASENZA AZINDUA TAWI JIPYA LA ACCESSBANK MJINI IRINGA


Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Meneja wa Tawi la AccessBank Iringa, Frederick Masungwa wakati wa uzinduzi wa tawi hilo hivikaribuni. Kushoto ni Mkuu wa Maendeleo ya Biashara wa benki hiyo, Andrea Ottina.

Kutoka kushoto, Mkuu wa Maendeleo ya Biashara wa AccessBank Andrea Ottina, Meneja wa Tawi la AccessBank Iringa Frederick Masungwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza wakikata keki wakati wa uzinduzi wa tawi la benki hiyo mjini hivikaribuni.


Mkuu wa Maendeleo ya Biashara wa AccessBank Andrea Ottina (kushoto) akilishwa keki Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza wakati wa uzinduzi wa tawi la benki hiyo mjini Iringa hivikaribuni. Katikati ni Meneja wa Tawi la AccessBank Iringa Frederick Masungwa.


Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza (mwenye kilemba) akiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa AccessBank, baada ya kuzindua tawi la benki hiyo mjini Iringa hivikaribuni.

MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amezindua tawi jipya la ACCESSBANK mjini Iringa, linaloifanya benki hiyo iwe na matawi 13 katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkuu wa maendeleo ya biashara wa benki hiyo, Andrea Ottina alisema ufunguzi wa tawi la benki hiyo mjini Iringa ni ushahidi wa dhamira yao ya dhati ya kutoa huduma bora kwa wateja wao nchini.

“Pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja wetu, tunataka wapate huduma zetu kwa wakati pamoja na kuimarisha urahisi wa huduma za kibenki,” alisema.

Ottina alisema Iringa ni miongoni mwa mikoa inayokua kwa kasi nchini kutokana na upatikanaji wa vivutio vingi, uwekezaji na uzalishaji wa chakula cha mazao ya biashara.

Alisema benki hiyo itaendelea kupanua huduma zake ili kufikia sehemu kubwa ya wateja nchini kote, pamoja na kuanzisha bidhaa na njia mpya za upataji huduma.

“Njia hizo ni kama vile huduma za kibenki kupitia simu ya mkononi na wakala wa kibenki ambao wamelengwa zaidi katika maeneo ya vijijini na mijini pia,” alisema.

Akizundua tawi hilo, Masenza aliipongeza benki hiyo kwa kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma bora za kifedha katika mkoa wa Iringa.

“Natoa wito kwa wakulima na wajasiriamali, wafanyabishara wakubwa na wadogo kuchukua faida ya huduma zinazotolewa na benki hii kama fursa ya kuendeleza shughuli zenu za kilimo na biashara,” alisema.

Alisema sekta ya benki ni muhimu katika maendeleo ya Taifa kwani ndiyo inayowezesha uwekezaji unaoweza kuleta mabadiliko kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Matarajio yangu ni kuona mnaendelea kutoa huduma itakayokuwa na mfuto, msiwe sehemu ya wale wanaonyanyasa wananchi katika utoaji wa huduma za kifedha,” alisema.

Awali Meneja wa tawi la AccessBank mkoani Iringa, Frederick Masungwa alisema benki hiyo ilianza kutoa huduma zake za kifedha mkoani hapa, Julai mwaka huu na hadi Novemba mwaka huu ilikuwa na wateja zaidi ya 3,000.

Masungwa alisema benki hiyo inatoa huduma za akaunti mbalimbali ikiwemo ya akiba, kikundi, hundi, amana, mikakati, wanafunzi, wafanyabishara wakubwa; na pia inatoa huduma za kutuma fedha ndani na nje ya nchi na huduma ya ATM kupitia Umoja Switch.

Alisema tangu waanze kutoa huduma hizo,katika kipindi cha miezi sita iliyopita mkoani Iringa wamekwishapata wateja zaidi ya 3,000.

AccessBank ni taasisi ya kifedha inayolenga kutoa huduma za kibenki kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kupitia wanahisa wake wa kimataifa ambao ni AccessHolding, International Finance Corporation, African Development Bank na MicroVest.

COMMENT HERE

SHARE